Nafasi ya Mwanamke katika ngano za Kiswahili

June 11, 2018 | Author: Sebastian Mbwillow | Category: Documents


Comments



Description

Nafasi ya Mwanamke katika ngano za Kiswahili Na Shaibu Issa Champunga Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Mei 2018

01 UTANGULIZI Kazi hii inahusu nafasi ya mwanamke katika ngano za Kiswahili. Ngano ni mojawapo ya kipera cha hadithi katika utanzu wa fasihi simulizi, vipera vingine katika utanzu wa hadithi ni visasili, tarihi pamoja na visakale. Na istilahi ya mwanamke katika kazi hii tunaifafanua kuwa, ni mtu mwenye jinsi ya Kike. Katika kuifanya kazi hii zitafafanuliwa istilahi muhimu zilizobebwa na swali letu ambazo ni dhana ya ngano na ngano za Kiswahili kutokana na mitazamo ya wataalamu mbalimbali na kisha kutoa tafsiri hizo kulingana na mtazamo wa kazi hii. Baada ya hapo tutajadili nafasi ya mwanamke kupitia ngano za Kiswahili kwa kumwangalia jinsi alivyochorwa kuwakilishwa katika mitazamo mbalimbali ya kijamii.

02 Fasili ya dhana Mulokozi (1989) anaeleza kuwa ngano (hurafa, vigano) ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Anaendelea kueleza kwamba utanzu huu unajumuisha fani kadhaa kwa mfano Istiara, Mbazi na Kisa. Akifafanua fasili hiyo Samwel (2015) anasema, ngano hutumia viumbe na vitu vingine visivyo na uhai kama wahusika, ndege na wadudu. Muhando na Basilidya (1976) wanaeleza kuwa ngano ni aina maalumu ya hadithi ipatikanayo katika fasihi asilia ya jamii yetu, fasihi ambayo ilitumiazaidi akili na ubongo wa binadamu kwa kuhifadhiwa kwake. Wanaendelea kueleza kuwa ngano nyingi aghalabu ni fupi na kutokana na ufupi huo, hizi si hadithi zinazozungumzia mambo kwa undani sana. Hadithi hizo huingia moja kwa moja katika kulitoa wazo kuu, na kila kipengele kijengacho ngano kama vile wahusika, vielelezo na mizungu mingineyo huelemea katika wazo hilo (Msokile 1992:8). Kutokana na fasili hii neno asilia linatudhihirishia kwamba chanzo cha ngano ni jamii husika. Kwa mfano katika jamii za Kiafrika ngano zitahusu jamii za Kiafrika

zinazoonesha ujasiri, uvumilivu uchapakazi na kujitoa muhanga pamoja na wakati mwingine huonesha udhaifu wa baadhi ya wanajamii. Msokile (1992:6) akimnukuu Esenwein anafasili ngano kuwa ni masimulizi yaliyorahisishwa. Kwa kawaida masimulizi hayo ni mafupi yasiyo na muundo kama wa hadithi za kawaida. Masimulizi hayo hutumia wahusika bapa na hutegemea matakwa ya fanani katika kujenga vitendo mbalimbali kuliko muundo katika kuwajenga wahusika. Katika fasili hii Esenwein anaonesha utendaji wa fanani kuwa ni jambo la msingi katika usimulizi wa ngano kuliko kuegemea katika muundo. Aidha Senkoro (1982) anasema ngano niutanzu wa Kifasihi simulizi ambao ulipitishwa toka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia yamdomo. Ngano kama kazi zingine za fasihi simulizi, zilikuwa na matumizi yake maalumu ya wahusika. Mwanzoni zilitumia wanyama, wadudu, miti mashetani, mazimwi kuwa wahusika wake wakuu. Zilipozidi kukua ziliingiza wahusika wa kibinadamu ijapokuwa bado wahusika hao walichanganyika na viumbe wengine pamoja na Miungu. Kutokana na mtazamo wa kazi hii inafasili ngano ni masimulizi yanayorithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, masimulizi hayo yahusuyo maisha ya kila siku ya wanadamu. Wakati mwingine masimulizi kuhusu mambo yasiyoonekana kama vile hadithi za mazimwi na zinazohusu mizimu lakini zikilenga kuonesha kuwa matendo hayo kwa kawaida kutokea kwa wanadamu. Vilevile masimulizi mengine huhusu wanyama ambao wanakuwa na tabia za kibinadamu wenye hisia za kweli, wenye mapungufu. Tunapozungumzia binadamu wenye mapungufu tunawalenga wahusika ambao wanakuwa rahisi kushindwa wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali. Kutokana na fasili hii ninakubaliana na Msokile (kashatajwa) kwamba chanzo cha ngano ni jamii husika. Kwa hiyo katika jamii ya Waswahili ngano zitahusu mila na desturi za jamii hizo. Kwa mantiki hiyo, Ngano ya Kiswahili ni masimulizi yapatikanayo katika fasihi asilia ya jamii ya Waswahili. Na waswahili katika kazi hii tunanaweza kusema; ni mtanzania au mkenya yeyote yule ambaye ni mweusi na hajachanganya damu na taifa lolote. Baada ya kuangalia fasili za ngano na maana ya mswahili kwa ufupi, nitatumia ngano za bara(Kigogo) na za pwani(Kizanzibari) kujadili nafasi ya mwanamke. Kama nilivyosema awali katika fasili, kuwa maudhui ya ngano ya Kiswahili huhusu waswahili ambapo kwa namna fulani hueleza na hujadili mila na desturi za waswahili. Hivyo nafasi ya mwanamke

imechorwa kwa namna tofautitofauti, yaani amechorwa kwa upande hasi na chanyakatika ngano za Kiswahili. 03 Nafasi chanya alizojengwa mwanamke katika ngano ya Kiswahili. Mwanamke kama mkombozi, Mwanamke anachorwa kama ni mkombozi wa matatizo mbalimbali yanayojitokeza katika familia, kwa mfano ngano ya “Umoja” kulikuwepo na watoto wawili wa kiume na wa kike ambao walifiwa na wazazi wao wawili, baada ya kukaa muda mrefu wakaishiwa chakula. Mtoto wa kiume akaondoka akaenda kutafuta chakula, akafika nchi moja akakutana na Bi kizee. Akamwelezea shida yake iliyomfanya hadi afike pale kwa Bibi kizee. Bibi akamwambia, Ewe mjukuu wangu, nirambe tongo nikuone. Yule mtoto akafanya alichoambiwa. Bibi akamuonesha nyumba kubwa ya Kifalme amabayo anaishi Zimwi, kuna vyakula na mali nyingi, lakini nenda majira ya saa12 huondoka kwenda kuchunga, panda ghorofa ya juu utapata chakula.Baada ya kwenda, alikikuta chakula katika magala, na kilichopikwa, na akala kile kilichopikwa na akajificha ndani ya jumba, aliporejea Zimwi alikuta chakula kimeliwa alipomuuliza kijakazi hakufahamu kwamba chakula kimeliwa na nani, akamuadhibu kwa kumchoma moto kijakazi wake, alipomwona anaungua huruma ikamjia yule Zimwi na kutaka kuuzma ule moto, ila moto ukamzidi naye Zimwihadi walikufa yeye na kijakazi wake. Kwa hiyo Mtoto alifurahi na kuenda kumchukua mdogo wake na yule Bibi Kizee wakaishi kwenye jumba lile. Kwa hiyo tunaona mwanamke amechorwa km mkombozi na hili linajitokeza hata katika jamii zetu, endapo tukiwa watiifu na kupenda na kushirikiana na wanawake tutapata mafakio. Mwanamke amechorwa kama mtu mwema mwenye huruma,hapa amechorwa kama mtu mwenye huruma baada ya kufanyiwa ubaya na mwanamme kijakazi na mumewe na baadaye akaamua kumsaidia bila kujali ubaya aliofanyiwa. Kwa mfano; kisa cha “Mwanamke mganga wa macho”. Mwanamke mmoja alikuwa akiishi na mumewe na mtumishi wa mumewe, mara nyingi mumuwe alikuwa akisafiri muda mrefu, yule mtumishi akamuhitaji kimapenzi, mwanamke akakataa, baada ya kukerwa kwa muda mrefu, na kutishiwa uhai akaamua kutoroka ili kuokoa uhai wake kwani alitishiwa kifo. Baada ya kuondoka huku nyuma yule mtumishi akapofuka macho. Aliporejea mume wa mke aliyetoroka, akamuuliza mke wangu yu wapi? Akasema sijuwi mimi si unaniona sioni? Katika safari yule Mwanamke alifika kwenye mti mkubwa akalala, usiku alitunukiwa uganga wa macho kwenye ndoto, akawa mganga wa akaanza kutibu hadi yule mtumishi wa mfalme akaja kuomba kutibiwa, yule Bibi

hakusita akamtibu na wala hakulipiza ubaya aliotendewa.Hapa tunaona pia Mwanamke amechorwa kama mwenye huruma na mwepesi kusamehe. Mwanamke kama mzazi na mlezi bora na mwaminifu. Katika ngano hizi mwanamke kama mlezi, mama wa mji na mwenye kuwajibika katika kuwatunza watoto na mume wake.Majukumu haya yamejidhihirisha katika ngano ya Kisa cha Zubeida msichana wa kwanza’. “Watu wageuka kuwa mawe”. Kwa muda wa miaka mingi baba yangu hakujaaliwa kupata mtoto mpaka nilipozaliwa mimi wakati akiwa ana umri wa uzee. Kwa hiyo, alinilea vizuri na kwa uangalifu mkubwa sana mpaka nilipofikia umri wa miaka sita. Kwa bahati mzuri katika kasiri yetu mulikuwa na bibi mzee aliyemuamudu Allah na aliyeamini kuwa Muhammad (s.a.w) ndiye mtume wa mwisho wa Allah. Baba yangu alimwamini sana ajuza huyu kwa wema, tabia na ujuzi wake wa mambo mengi lakini hakuna aliyeijua siri ya Imani yake. Kwa hiyo baba yangu alimtunukia heshima na ukarimu mkubwa akiamini bibi huyo ana Imani kama yao. Nilipotimiza umri wa miaka sita baba akanikabidhi kwa yule bibi anielimishe na anifundishe dini yao. Yule bibi akanipokea kwa mikono miwili, akanifundisha dini ya Kiislamu: namna ya kutawadha na kuswali swala za faradhi na za sunna. Akanifundisha vilevile Qurani tukufu na Hadithi na yote aliyoyajua akinionya nisimwambie yoyote juu ya Imani yangu- hata baba yangu- kwani akijua ataniua! Baada ya muda yule bibi akafariki dunia. “Siku moja wakati wakazi wa jiji walipokuwa katika harakati za dini yao”, sauti kama radi ikasikika kote ikisema, “Watu wa jiji hili, achene kuabudu moto abuduni Mwenyezi Mungu, subbbhanahu wa Ta’ala”. Wakiwa wamejaa na hofu kubwa, wakazi wote wakaelekea kwenye kasri la baba yangu kutaka kujua maana ya ile sauti: lakini baba yangu akawaambia wasiogope akisisitiza wasiache Imani yao. Baada ya kutubu, wakafuata ushauri wa baba yangu. Basi baada ya mwaka mmoja, wakati wakiendelea na ibada yao ya uwongo, ile sauti ikasikika tena. Ikaendelea kufanya hivyo ndani ya muda wa miaka mitatu,kila mara ikisikika siku ileile na wakati uleule. Hata hivyo wakazi wa jiji hili hawakujali; wakaendelea tu kuabudu moto mpaka asubuhi moja, kulipokucha, ghadhabu za Mwenyezi Mungu zikawashukia kutoka mbingunina wote waliokuwemo katika jiji hili, pamoja na hayawani wote, wakageuka kuwa mawe meusi kama ulivvyowaona; mimi peke yake ndiye niliyeokoka. Kwa hiyo hapa

tunaona katika simulizi hii mwanamke amechorwa kama mtu mwema mwenye kufuata maadili mema. Mwanamke kama mvumilivu wa matatizo na shujaa.Katika ngano hizi taswira ya mwanamke imeonekena kama shujaa katika jamii yake. Kwa mfano ngano ya jamii ya Kigogo yenye anuani ya; “Mama aliyenyang’anywa mtoto na Kima” Hapo kale palikuwa na mama mmoja na mtoto. Basi mama akawa anaenda na mtoto wake shambani halafu mtoto anamuweka chini ya mti naye anafanya kazi yake, baada ya kukataliwa na ndugu wa mume kumsaidia kumlea akiwa anafanya kazi yake. Hivyo basi ilikuwa kawaida Kima huja kucheza na yule mtoto hadi wakazoeana. Siku moja Kima alipokuja alicheza na mtoto, alipoona mama mtu hamwangalii akambeba mtoto akatoroka naye. Mama akaanza kumtafuta mtoto, akasafiri safari ndefu. Akatembea akakutana na wanyama akawauliza, wakasema endelea na safari akakutana na ndege, hadi viumbe wasio kamili watu wenye mkono mmoja, jicho moja moja, pua za upande, sikio moja moja akawauliza akaambiwa endelea na safari…..Mwisho amefika penye maji, akamkuta Bi kizee amekaa ukingoni anaota jua. Bibi Kizee mchafu mwenye tongo mbichi na kavu za kijani zenye rangi za usaha hajanawa siku nyingi sana. Akamuuliza mahali ambapo angepata mtoto wake, Bibi Kizee akasema, “nilambe kwanza tongo tongo hizi ili macho yangu yaone vizuri ndipo nikuelekeze njia”. Mwanamke akawa anafanya alichoambiwa, anamlamba Bi kizee tongotongo zote bila kutema kuonyesha kinyaa zikaisha zote. Bi kizee akambeba yule Mwanamke mgongoni wakaingia majini na kuogolea hadi kilindini. Chini kabisa akakuta jumba kubwa sana ajuza akamwashiria kuingia ndani. Alipoingia ndani bibi akasema “uende pale penye vyungu ukivikuta piga vinavyolia “nge nge nge”, usifunue kinacholia “mbu mbu mbu” akaenda akafanya hivyo. Akamkuta mtoto wake humo, kulembwa, kapendeza ajabu. Akamchukua, Bibi akambeba tena na kuwarudisha nchi kavu wakaagana mama na mtoto wakaondoka kurudi kwao (Balisidya 1997). Licha ya kumuona kuwa mwanamke ni shujaa na mvumilivu wa matatizo, katika ngano hii pia tunamuona mwanamke kachorwa kama mtu mtiifu. Baada ya kutii masharti mbalimbali ili aweze kufanikiwa lengo lake. Mwanamke kama mtu mwenye miujiza, mwanamke huchorwa kama mtu mwenye miujiza anayeweza kulitenda jambo ambalo kwa fikra za kawaida haliwezekani, kwa mfano katika ngano ya “Mama aliyenyang’anywa mtoto na Kima” hii ni ngano ya kigogo ambayo inamchora bibi kizee alivyomsaidia mama aliyepotelewa na mtoto, Bibi kizee huyo alimchukua yule mama wakaingia majini na wakamkuta mtoto chini ya maji amehifadhiwa

vizuri kwenye maji. Hii ni miujiza ambayo kwa mazingira ya kawaida mambo haya hayafanyiki na hayawezekani. Mwanamke kama mtu mwenye akili, kwa mfano katika simulizi ya “watoto saba” (senkoro 1997:347) Hapo zamani za kale walikuwepo mtu na mkewe. Watu hao wakazaa watoto wao saba. Kitinda mimba kwa bahati mzuri akawa ni mwanamke ambaye ni mmoja tu. Sasa kwa bahati mbaya yule mama mzazi akapatwa na maradhi na akafariki dunia. Akabakia yule baba mzazi. Alipokaribia kufa akawaita wanawe wote na akawausia kwa kusema “Yule mtoto anayetaka mali na aniambie: na anayetaka radhi yangu aniambiye vili vile”. Kwa hiyo wale watoto wakainama chini muda mrefu kidogo. “Sisi tunataka mali”, wakajibu vijana sita wa kiume. Akabakia yule msichana ambaye ni kitinda mimba, nae akasema. ‘Mie nataka radhi yako”. Sasa mzee akawauliza wale wanaotaka mali, hamtagombana na huyu mwenzenu anayetaka radhi? Wakajibu, “hata hatutagombana na mtu”. Kwa hiyo yule mzee baada ya kufika siku zake alikufa. Sasa wenye kutaka mali walichukua mali, yule msichana mwenye kutaka radhi, siku moja ilimshika njaa kali akaenda shambani kwa kaka zake kukata mua na kutafuna bila kuwaomba kaka zake, na alifanya hivyo kwa siku ya pili. Kaka yake mmoja akauliza nani kakata mua? yule binti akajibu ni mie. Akasema yule kaka, kama ni wewe ngoja nikutie adabu! “Ilivyokuwa umeikata miwili na weye nataka kuikata mikono yako yote.” Yule msichana masikini ya Mungu mikono ikakatwa ikabakia mapigi matupu na nyumbani wakamfukuza. Yule msichana alifanya safari ya kuhama na kuelekea mbali. Huko alifika upenyuni mwa nyumba moja. Na alichukuliwa na mfalme mmoja na kumuoza kwa mwanawe. Mtoto wa mfalme, akawa anaishi naye kwenye jumba la kifalme. Kwa hiyo wale waliotaka mali ikawa wamekuwa masikini hawana chochote mali yote wameharibu. Na yule msichana akawa tajiri na kujulikana ulimwengu mzima yeye na mumewe. Akawa hana shida tena kwani anatumia radhi za wazee wake. Hivyo basi ngano hii inatuonesha kwamba mwanamke ni kiumbe mwenye akili sana za maisha na anayetambua thamani ya utu katika maisha ya mwanadamu, aliwathamini wazazi akaishi nao kwa kupata radhi ndipo akafanikiwa. Hata hivyo kupitia ngano hii tunamuona mwanamke amechorwa kama mtu anayeweza kumiliki mali katika jamii. (Kiuchumi). Ingawa katika jamii suala hili limepuuziwa sana na kumuona mwanamke kama mtu ambaye hawezi kumiliki mali, kwa hiyo jambo la msingi ni

kutoa elimu juu ya umma kwani kila mtu ana nafasi ya kumiliki mali bila kujali tofauti ya kimazingira. Kwa hakika hizi nafasi chanya alizojengwa mwanamke katika ngano ndizo zilizotakiwa zichukuliwe na jamii mzima bila wao wanawake wenyewe kujisahau katika kuwa mstari wa mbele katika shughuli za kimaendeleo. Laikini kutokana na tamaduni za Waswahili na dini zilizoletwa na wageni (Ukiristo na Uisilamu) zimechangia kushusha hadhi ya mwanamke na kumuona kama kiumbe duni katika jamii, asiyeweza kujitegemea katika maamuzi, kiuchumi na hata katika masuala mbalimbali ya kijamii. Huu ni mtazamo hasi katika jamii na kwa kulijadili hili tutatumia ngano za Waswahili.

04 Nafasi hasi alizochorwa mwanamke katika ngano za Kiswahili. Mwanamke kama mtu mwenye wivu. Kwa mfano: Katika ngano mwanamke anachorwa kama mtu mwenye wivu na asiyependa maendeleo ya mwenziwe kiuchumi na kijamii, katika ngano hii anaoneshwa wivu wa kimapenzi. “Kisa cha Msichana Lozi”. Katikanchi moja kulikuwapo tabia ya kuchonga meno, hasa kwa wasichana. Katika mji mmoja, kulikuwa na msichana mmoja aliyeitwa Lozi. Siku moja wasichana wa mji huo walikwenda safari kwa udhuru wa kuchonga meno kwani mabingwa wa kuchonga meno walikuwa wachache. Katika msafara huo Lozi naye alikuwamo walipofika huko kwa wachonga meno, walihudumiwa wote lakini kati ya wote aliyechongwa meno vizuri sana alikuwa Lozi, Lozi msichana wa watu akapendeza mno, wasichana wenzake, wakaanza kumwonea wivu kwa vile alikuwa kachongwa vizuri mno kuwapita. Na kutokana na wivu huo, ndipo wasichana wengine walipopanga njama za kuhujumu uhai wa Lozi. Waliona kwamba endapo watafika wote kule mjini kwao basi labda Lozi atawahi hasa kupata wavulana. Wakiwa njiani kurudi hivyo, wote kwa pamoja wakamshika Lozi na kumtumbukiza katika bwawa, akafa. Walipofika nyumbani mjini kwao wakaulizwa wapi wamemwacha Lozi; wao wakajibu kwamba hawakufika naye mbali. Wakaeleza kwamba wakiwa njiani, Lozi alionekana kuchoka. Hivyo akaamua mwenyewe kurudi nyumbani siku hiyohiyo……. hatimaye alitafutwa Lozi lakini akakutwa amekufa ndani ya maji.

Pia katika kisa hiki tunaona kwamba mwanamke amechorwa kama msaliti na ni mtu mwenye rohombaya, wasichana hawa wanadiriki kupoteza uhai wa mwenzao kwa ajili ya kumuona kapendeza kuwazidi. Pia katika ngano hii tunaona mwanamke kachorwa kama mwenye kupenda anasanaurembo (chombo cha starehe) katika maisha ili wapendwe na wanaume. Mwanamke ni mtu mwenye tamaa, ‘tamaa’ ni hamu kubwa ya kutaka kupata kitu. Katika nganohiiMwanamke kachorwa kama mtu mwenye tamaa ya kutakakupata kitu bila ya kufanyia kazi.kwa mfano; “Kisa cha Msichana na Jini”. Hapo zamani za kale, vijana fulani walizoea kwenda kucheza ngoma nyakati za usiku. Ngoma yao ikavuma sana hata ikawa kwamba vijana vijiji vingine wakawa wanahudhuria. Wachezaji wakawa wengi siku hadi siku na wale waliokuwa hodari wakawa na bahati ya kupendwa sana na wasichana. Siku moja kijana mmoja ambaye alikuwa mgeni kabisa katika sehemu hiyo alifika. Kijana huyo akaonesha mchezo mzuri ambao hujawahi kuchezwa katika sehemu hiyo. Akacheza vizuri na kwa ufundi mwingine na wachezaji wote wakabaki kumwangalia yeye tu. Ngoma ilipomalizika wasichana wawili warembo wa sehemu hiyo wakaamua kumfuata kijana huyo ambaye ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kufika hapo na tena hawamfahamu. Wasichana wale walimfuata na kwenda naye hadi kwake. Kumbe kijana huyo hakuwa binadamu; ila alikuwa jinni mla watu…….” Nyumbani kwa kijana huyo ambapo palikuwa porini sana alikuwepo bibi kizee mmoja akimshughulikia jinni katika shughuli zote zinazohusu binadamu apatapo watu kama hao. Bibi kizee alipowaona wasichana hao jinsi walivyokuwa wazuri, aliwasikitikia sana, maana alikuwa akijua ya kwamba baada ya muda si mrefu lazima wataliwa. Jini alipoondoka kwenda mawidoni, bibi kizee aliwaeleza vijana wale habari ya jinni hilo. Wasichana wakaogopa sana na wakamuomba bibi kizee awasaidie. Bibi kizee akawaambia ya kwamba hakukuwa na namna nyingine yoyote ila kutoroka tu…..Hatimaye walifanikiwa kutoroka. Hapa tunaona katika ngano hii tunaoneshwa kuwa wanawake ni viumbe wenye tamaa iliyokithiri kiasi kwamba wanakubali kwenda kuishi kimapenzi na mtu wasiyomfahamu.

05 Hitimisho Kimsingi kazi nyingi za fasihi za zamani na hadi sasa, ngano ikiwemo, zinaonesha zinamkandamiza mwanamke, kwa hiyo tunatakiwa kusoma upya kazi za kifasihi ili kusisitiza vipengele vilivyopuuzwa na waandishi wa awali huenda waliandika kutokana na utamaduni. Kwa sasa tunasisistiza kuunda upya mfumo wa kupigania haki za wanawake ili kuleta ukombozi kwa wanawake, pamoja na kupinga miundo ya kijadi ya kumkweza mwanaume na kumdunisha mwanamke. Tunatakiwa kujenga jamii mpya yenye misingi katika amali za binadamu bila kujali tofauti za kimaumbile. Piawatunzi mbalimbali wa kazi za fasihi wanatakiwa kuwachora wahusika wanawake kama kielelezo cha wenye uwezo katika jamii kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Kuamsha na kuzindua mwamko miongoni mwa wanawake ili wawe watendaji zaidi na washiriki ipasavyo katika ukombozi wao wenyewe wasio wategemea wanaume kujitambulisha. Hata hivyo hali ya maisha ya binadamu ni zao la mahusiano ya kijamii ambayo huendelezwa na kubadilishwa na jamii husika. Hivyo basi jamii inatakiwa ibadilike kwa kuweka misingi katikaamali za binadamu kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa bila kujali tofauti za kimaumbile.

MAREJEO Adam, H. (2004) Masimulizi ya Alfu lela U lela au Siku Elfu Moja na Moja. Kitabu cha pili. Dar-es-Salaam: Mkuki na Nyota Publishers Ltd. Balisdya, M. L. Y. (1997) Mabadiliko katika Fasihi ya Wagogo. Tasnifu ya Umahili (Haijachapwa). Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Muhando, P. na Balisdya, N (1976). Fasihi na Sanaa za Maonyesho. Dar es Salaam. TUKI. Mulokozi, M. M. (1996) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili: Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria. Msokile, M. (1992) Misingi ya Hadithi Fupi: Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Senkoro, F. E. M. K. (1997) The Significance of the Journey in Fold Tales from Zanzibar. Tasnifu ya Uzamivu (Haijachapwa). Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Senkoro, F.E.M.K (1982) Fasihi: Press and Publicity centre, Dar es Salaam.

Copyright © 2024 DOKUMEN.SITE Inc.